ZARA TOURS YANG'ARA TENA KWENYE TUZO ZA SERENGETI, NA KUPANUA MFUMO WAKE WA HESHIMA ZA KIMATAIFA


Kampuni ya utalii ya Zara Tours ya mjini Moshi kwa mara nyingine imethibitisha uongozi wake katika sekta ya utalii nchini Tanzania baada ya kujinyakulia tuzo nyingine ya heshima kwenye tuzo za Serengeti, na kuendeleza msururu wa heshima ambao kampuni hiyo imekuwa ikijipatia karibu kila mwaka. 


Tuzo hiyo ni miongoni mwa tuzo 51 zilizotolewa wakati wa hafla ya utoaji wa tuzo za Serengeti iliyofanyika usiku wa kuamkia jana kwenye hoteli ya Mount Meru jijini Arusha, hafla iliyowakutanisha wadau wakuu wa utalii kutoka Tanzania na nje ya nchi.

 

Naye Mgeni Rasmi Waziri wa Fedha Dkt.Mwigulu Nchemba ameipongeza sekta ya utalii kwa mchango wake mkubwa katika kukuza uchumi wa taifa, kutengeneza fursa za ajira na kuitangaza Tanzania duniani.

Akizungumza mara baada ya kukabidhiwa tuzo hiyo, Mkurugenzi wa Zara Tours, Bi. Zainabu Ansell alisema mafanikio hayo yanadhihirisha uchapakazi, ari ya pamoja na ushirikiano wa karibu kati ya serikali na wadau wa sekta binafsi hususan katika ulinzi na uendelezaji wa vivutio vya taifa kama vile Mlima Kilimanjaro. 


“Mafanikio yanayoonekana ya Mlima Kilimanjaro ni ushahidi tosha wa kazi kubwa inayofanywa na serikali kwa kushirikiana na wadau wa utalii,” alisema Bi Zainabu. "Mazingira ya mlima yameboreshwa sana, huduma zimeimarishwa, na usalama umeongeza sana kuwapa wageni uzoefu wa kipekee." 



Aliongeza kuwa maboresho haya yameendelea kuinua Mlima Kilimanjaro kama alama ya kimataifa, na kuiweka Tanzania kama moja ya sehemu zinazoongoza kwa utalii wa mlima Afr. na duniani kote.


Kwa mujibu wa mkurugenzi huyo, kuongezeka kwa idadi ya wapanda mlima Kilimanjaro kumekuza kwa kiasi kikubwa sekta ya utalii na kuongeza pato la taifa huku makampuni kama Zara Tours yakichangia pakubwa katika kuhakikisha wageni wanapata huduma za kiwango cha kimataifa.

 "Ninajivunia sana mafanikio haya.

 Leo ni siku ya kusherehekea jinsi tumefika," alisisitiza. "Mimi na timu yangu tumejitolea kikamilifu kuinua viwango vya kitaaluma, kukumbatia uvumbuzi, na kuvutia wageni zaidi kupata uzoefu wa kupanda Mlima Kilimanjaro." 


Bi. Zainabu alisisitiza dhamira ya Zara Tours ya kuendelea kuwa mshirika wa karibu wa serikali katika kukuza utalii endelevu, uhifadhi wa mazingira, na kuiweka Tanzania kwenye majukwaa ya utalii ya kimataifa. Tuzo za Serengeti zinalenga kutambua na kuenzi taasisi, makampuni na watu binafsi waliotoa mchango mkubwa katika kukuza na kuendeleza sekta ya utalii nchini Tanzania.




Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

WAGOMBEA,WANACHAMA WA CCM VILIO JUU YA KURA ZA MAONI HAI

BARAZA LA ARDHI LAFUTA KESI YA ARDHI KUTOKANA NA DOSARI ZA KISHERIA

TAWIRI YAWAKARIBISHA WADAU KUFANYA TAFITI KATIKA SPISHI MUHIMU YA SOKWE