MEYA WA JIJI LA ARUSHA AELEZA MAFANIKIO YA ZIARA YA WAZIRI WA TAMISEMI KATIKA KUKAGUA MIRADI YA MAENDELEO.


Meya wa Jiji la Arusha, Mheshimiwa Maximilian Iranque, amezungumzia kwa kina ziara ya kikazi ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – TAMISEMI, Profesa Riziki Shemdoe, iliyofanyika jijini Arusha kwa lengo la kukagua na kutathmini utekelezaji wa miradi ya maendeleo inayotekelezwa na Jiji hilo.


Katika ziara hiyo, Profesa Shemdoe alitembelea na kukagua miradi mbalimbali ya kimkakati ikiwemo ujenzi wa Soko la Kilombero, uwanja wa mpira, pamoja na jengo la Utawala la Jiji la Arusha. Waziri alipata fursa ya kujionea hatua kubwa zilizofikiwa katika utekelezaji wa miradi hiyo, ambayo inalenga kuboresha huduma kwa wananchi na kuchochea maendeleo ya kiuchumi katika jiji.


Akizungumza baada ya ziara hiyo, Meya Iranque amesema kuwa Waziri wa TAMISEMI ameridhishwa na kasi, ubora pamoja na usimamizi wa miradi hiyo, akisisitiza kuwa miradi hiyo ina mchango mkubwa katika kuinua uchumi wa Jiji la Arusha, kuongeza fursa za ajira kwa wananchi, pamoja na kuboresha mazingira ya biashara na utoaji wa huduma za kijamii.


“Mhe. Waziri ameridhishwa sana na hatua tuliyofikia. Miradi hii ni muhimu kwa maendeleo ya wananchi wetu na itaongeza mapato ya jiji pamoja na kuboresha maisha ya wakazi wa Arusha,” amesema Meya Iranque.


Aidha, Meya huyo amewashukuru wataalamu, wakandarasi pamoja na wadau wote wanaoshiriki katika utekelezaji wa miradi hiyo kwa ushirikiano wao mzuri na uzalendo, akisisitiza umuhimu wa kuendelea kufanya kazi kwa viwango vinavyokubalika.


Kwa upande mwingine, Meya Iranque ameahidi kuwa Jiji la Arusha litaendelea kusimamia kwa karibu utekelezaji wa miradi yote ya maendeleo ili kuhakikisha inakamilika kwa wakati, kwa ubora unaotakiwa na kwa kuzingatia malengo ya Serikali pamoja na matarajio ya wananchi wa Jiji la Arusha.














Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

WAGOMBEA,WANACHAMA WA CCM VILIO JUU YA KURA ZA MAONI HAI

BARAZA LA ARDHI LAFUTA KESI YA ARDHI KUTOKANA NA DOSARI ZA KISHERIA

TAWIRI YAWAKARIBISHA WADAU KUFANYA TAFITI KATIKA SPISHI MUHIMU YA SOKWE