UKATILI WA KIJINSIA KILIMANJARO POLISI WAJA NA MKAKATI MPYA WA ELIMU
Jeshi la Polisi Mkoa wa Kilimanjaro limezindua kampeni mpya iitwayo "Tuwambie Kabla Hawajaharibiwa," ikiwa na lengo la kupambana na vitendo vya ukatili wa kijinsia dhidi ya watoto, ambavyo vimezidi kushika kasi katika mkoa huo.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Mkuu wa Dawati la Jinsia na Watoto Mkoa wa Kilimanjaro, Mrakibu wa Polisi Asia Matauka, alisema kuwa kampeni hiyo inalenga kuelimisha jamii juu ya namna ya kuzuia vitendo vya ukatili kabla ya kuathiri watoto.
“Tangu Januari hadi Agosti 2023, tulipokea kesi 415 za ubakaji na ulawiti, lakini mwaka huu kwa kipindi hicho hicho zimeripotiwa kesi 285. Hata kama idadi inaonekana kupungua, bado hali si salama. Tunahitaji kuendelea kutoa elimu ili matukio haya yasitokee kabisa,” alisema Matauka.
Alieleza kuwa baadhi ya matukio hayo yanachangiwa na imani za kishirikina ambapo wazazi au walezi huwafanyia watoto vitendo vya ukatili kwa matarajio ya mafanikio. Matauka alisisitiza umuhimu wa kuelimisha jamii ili kuondoa imani hizi potofu.
Kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Mkuu wa Wilaya ya Rombo, Raymond Mwangwala, aliipongeza Jeshi la Polisi kwa kuanzisha kampeni hiyo na kuizindua rasmi katika ukumbi wa Shule ya Polisi Moshi (TPS).
“Polisi wa zamani walikuwa wanaogopwa, lakini sasa polisi ni kimbilio la raia. Polisi wa sasa hawashughulikii tu kukamata wahalifu, bali wana jukumu la kusimamia maendeleo ya jamii na kutoa ushauri,” alisema Mwangwala.
Alieleza kuwa Jeshi la Polisi linafanya kazi kubwa ya kutoa elimu kwa jamii, kusaidia watoto walioko kwenye mazingira hatarishi, na kuwasaidia kwa kuwasiliana na taasisi zinazoweza kutoa msaada wa kisheria.
Mwenyekiti wa Shirikisho la Malezi na Ulinzi wa Jamii Tanzania Mkoa wa Kilimanjaro (SMAUJATA), Immaculata Mwigani, aliongeza kuwa shirika lake litaendelea kushirikiana na Jeshi la Polisi katika kampeni hiyo, licha ya changamoto ya ukosefu wa rasilimali.
“Hata kama hatuna magari wala pesa, tunafanya juhudi za kutembelea nyumba kwa nyumba kutoa elimu kwa jamii kuhusu madhara ya ukatili wa kijinsia. Changamoto kubwa ni wazazi kuwaachia watoto wao bila uangalizi, hali inayosababisha watoto hao kuwa katika hatari kubwa,” alisema Mwigani.
Jeshi la Polisi limesema kuwa kampeni hiyo inalenga kuwafikia vijana wa shule za sekondari na vyuo vikuu, ili kuhakikisha wanajitambua na kuepuka vitendo vya ukatili. Elimu itaendelea kutolewa katika maeneo yote ya Mkoa wa Kilimanjaro.
“Kampeni hii itatusaidia kwa kiasi kikubwa kuzuia ukatili kabla ya kuharibu maisha ya watoto wetu,” alihitimisha Mrakibu Matauka.






Maoni
Chapisha Maoni