POLISI WAONYA MADEREVA:MWENDOKASI NA ULEVI VYATAJWA KUSABABISHA AJALI NYINGI
Moshi. Mwendokasi umetajwa kuwa chanzo kikubwa cha ajali nyingi barabarani nchini, huku madereva wakionywa kuhusu matumizi ya vilevi na kutokuzingatia alama za barabarani.
Hayo yameelezwa leo alfajiri, Oktoba 17, 2024, na Mkuu wa Kitengo cha Elimu kwa Umma na Mafunzo kutoka Makao Makuu ya Kikosi cha Usalama Barabarani, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Michael Deleli, alipokuwa akizungumza na madereva katika Kituo Kikuu cha Mabasi Moshi, mkoani Kilimanjaro.
ACP Deleli amebainisha kuwa asilimia kubwa ya ajali barabarani zinasababishwa na makosa ya kibinadamu, akiwataka madereva kuendesha kwa uangalifu ili kuepusha ajali zinazogharimu maisha ya watu na Taifa kwa ujumla.
"Baadhi ya madereva wanatumia vilevi na kushindwa kuzingatia sheria za usalama barabarani, hali inayochangia ajali nyingi. Tunafanya zoezi la kupima ulevi kwa madereva ili kudhibiti hali hii," alisema ACP Deleli.
Aidha, aliwasisitiza madereva kuhakikisha wanatoa huduma bora kwa abiria wao ili kujenga uaminifu na kuepusha malalamiko yanayoweza kuharibu taswira ya kampuni wanazozifanyia kazi.
"Dereva mzuri ni yule aliyepitia mafunzo na anayefuata maadili ya kazi yake," aliongeza.
Kwa upande wao, madereva walilishukuru Jeshi la Polisi kwa kuwapatia elimu na mafunzo, wakiahidi kuyafanyia kazi ili kuboresha usalama barabarani.
"Tunaipongeza Polisi kwa kuwa karibu nasi na kutuongoza kwa njia sahihi," alisema mmoja wa madereva.
Wakizungumzia zoezi hilo, abiria waliokuwa wakisafiri kwa mabasi hayo walieleza kuridhishwa na elimu iliyotolewa, wakiomba jeshi la polisi liendelee kutoa elimu mara kwa mara ili kuepusha ajali zinazoweza kuepukika.






Maoni
Chapisha Maoni